Ni kipi ambacho Yesu alimaanisha kwa fumbo hilo “Mkumbukeni mkewe Lutu”? Ni kipi ambacho mwanamke wa zamani zile alikuwa nacho kama kielelezo kwa watu wanaotazamia kufungwa kwa historia? Kwa nini Bwana amhusishe mkewe Lutu na kipindi chetu? Yesu alimtumia kama onyo la kutisha. Mwanamke yule alizizima, asiye mwangalifu, na asiye mtiifu. Mwishowe hukumu za Mungu zilimwangukia, na akawa nguzo ya chumvi katika tambarare za Sodoma. Nafikiri kwamba moja ya hatari ya kutisha kwa watu wa Mungu katika siku za mwisho itakuwa kujitenga taratibu toka kwenye kweli vile alivyofanya mkewe Lutu. Yesu alionya kuwa ukosefu wa nguvu za kiroho unachukua nafasi pasipo kutambua: “Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa” (Mathayo 24:12).
Vile misukumo ya mapatano na makubaliano ya desturi inapofurika, imani hupungua na kutoweka taratibu. Ninakiri kwako kwamba hili leo ni tatizo linalomkanganyisha mno mchungaji. Pengine waongofu wapya wanapobatizwa na kujiunga na kanisa wanabubujikwa na ule uzoefu ajabu wa upendo wa kwanza. Wako radhi kwenda po pote na kufanya lo lote kwa ajili ya Bwana. Shauku yao inatia uchangamfu. Lakini punde mchungaji anagundua kuwa hamasa inaanza kufifia kidogo, na waongofu hao “hawachangamki tena na imani yao.” Taratibu wanaanza kupungua katika ushiriki na hata mahudhurio kanisani. Mchungaji huwatembelea na kujaribu kugundua tatizo. Kwa mshangao, anagundua kwamba bado wanaamini kama mwanzo, lakini wamepoteza upendo wao kwenye kweli. Tunauelezeaje ulegevu huu wa nguvu za kiroho? Ni kwa jinsi gani mwovu hunyang’anya moyo wa dhati wa uzoefu wa mkristo? Jambo moja ni hakika: haitokei papo hapo au kwa ghafla.
Watu hupoteza upendo wao kwa ile kweli hatua kwa hatua. Kidogo kidogo huidhoofisha misingi na huinajisi imani, mpaka inapotea kabisa isipokuwa utupu na ushika desturi tu. Baada ya kusoma yote ambayo Yesu alisema kuhusu wale wanaookolewa, tunaona ukweli mmoja adhimu na halisi ukionekana dhahiri. Mbinguni hakutakuwako na moyo uliogawanyika. Wakombolewa hawatajisalimisha nusu. Wale wanaoingia katika ufalme wa Mungu watakuwa pale kwa sababu walitaka uzima wa milele kuliko cho chote kile katika dunia hii. Bwana Yesu alimtumia mkewe Lutu kama kielelezo kwa wale ambao katika siku za mwisho hawatakuwa na lengo moja tu kwa ajili ya ile kweli; ambao watapenda zaidi mambo ya dunia hii kuliko mambo ya Mungu. Kristo alisema, “Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.” (Luka 14:33).
Je, unakumbuka kisa katika Biblia kuhusiana na mfanya biashara aliyekwenda akitafuta kito cha thamani duniani? Hatimaye alikipata na kugundua kuwa kilikuwa kikiuzwa. Lakini bei yake ilikuwa kubwa mno! Ili kuweza kuinunua lulu ile ilimpasa kuuza vyote alivyokuwa navyo na kutumia kila iliyokuwa akiba yake maishani. Lakini zingatia hili: Tamanio la mtu yule kwa ajili ya ile lulu lilikuwa la kina mno na lilimshurutisha kiasi cha kutokujadiliana kuhusu bei. Hakuona haja ya kusubiri mpaka atakapoweza kukidhi gharama. Wala hakujaribu kufanya makubaliano ya kupunguziana bei. Papo hapo na kwa hamu aliharakisha, akauza kila alichokuwa nacho, na kurudi na pesa kununua kito kile toka kwa mmiliki. Lulu, kwa hakika, ni ishara ya uzima wa milele, na wale wanaoutamani sharti wajitayarishe kuwekeza kila kitu walicho nacho ili kuupata.
Lutu alipewa uchaguzi wa uelekeo ambapo nchi yote ilikuwa mbele yake. Upande mmoja kulikuwa na milima iliyojawa kijanikibichi ikiwa na milima mirefu; upande mwingine ulielekea katika vituo vya biashara za bidhaa baina ya mataifa vyenye msongamano mkubwa. Mvuto wa vitu ulio katika miji hiyo tajiri ulikuwa na matokeo mujarabu kwa Lutu, na Biblia inaandika wazi kabisa kwamba, “akajongeza hema yake mpaka Sodoma” (Mwanzo 13:12). Mwelekeo wa kutarajika wa msiba wa siku za usoni uliandaliwa kwa uamuzi huo wa awali kuishi karibu na miji miovu. Lutu anasimama kama mtu wa makusudi mema. Ni dhahiri kwa hakika hakupanga kuichukua familia yake kuipeleka kwenye mazingira ya mjini ya Sodoma iliyojaa dhambi. Alipanga kuishi kwa ujirani tu, ambapo angejipatia faida ya fursa za kiuchumi za mji ule wenye pilikapilika za biashara.
Yumkini alikuwa akisita kuifanya familia yake iingiliane na wakazi wapotovu wa Sodoma na Gomora. Kwa kweli hakuwa na wazo kabisa la kuisalimisha dini yake. Lakini kulitokea nini pamoja na makusudi hayo makubwa? Maskini Lutu alimpoteza mke wake, mali zake, na karibu ayapoteze maisha yake. Makusudi mema bado hayakuwa mema vya kutosha. Taratibu alikuwa akiikaribia miji mpaka mwishowe aliingia kabisa kuishi pamoja na wenyeji wa Sodoma. Mipango yake kuyalinda matakwa ya kiroho ya watoto wake ilisongwa na tamaa ya vitu. Mawazo yake ya kimantiki kuhusu kuzuia uovu kwa ratiba shurutishi za maombi na dini ya madhabahu haikuonekana kufanya kazi kabisa kama alivyokuwa amepanga.
Taratibu aliingiliana na mazingira na aliwaangalia watoto wake wakiiga kidogo kidogo njia za majirani zao wamataifa. Nina hakika Lutu hakutulia pale alipokaa kwa mara ya kwanza miongoni mwa raia waovu wa mahali pale pa machukizo. Kila siku alisikia habari za kuenea kwa kiwango cha uhalifu. Lazima alichukia na hata kushtushwa na masihara ya kuchukiza na lugha chafu. Ndipo angepaswa kuwa mwangalifu kwa familia yake kuvutiwa na mtindo potovu wa maisha ya marafiki na majirani zao. Mwishowe, binti zake waliingia katika mahusiano ya kimapenzi na wanaume wa kidunia nao wakaolewa. Wakiwa mbali na nyumbani kwao, wakiwa wameungana na maadui wa Mungu, walipoteza imani yote ya dini yao ya zamani kipindi cha utoto na ujana wao. Walianza kumwangalia Lutu kama aliyeshikilia imani kupita kiasi na mwenye mawazo finyu na punde walidhihirisha uhuru wao mwingi uliotokana na maonyo ya moyo nusunusu ya baba yao kusimamisha ibada ya kweli nyumbani kwao.
Hata hivyo, huwa tuna mwelekeo wa kusikitika kuhusiana na Lutu katika majaribio yake ya kuvunja moyo katika kushikilia uhuru wa mke na watoto wake waliokuwa wamerudi nyuma. Alikuwa na mengi dhidi yake, lakini mengi ya hayo yalitokana na udhaifu na kusita kwake mwenyewe. Maridhiano ya mara hii yalizaa maridhiano mengine mpaka mwishowe alikuja kupotoka kabisa juu ya uasi wa familia yake ya kidunia.
Ibrahimu alikuwa akiwasilisha maombi na sadaka zake usiku na asubuhi kwa ajili ya familia ya mpwa wake. Je, ilikuwa ni kwa sababu hakukuwa na maonyo yo yote yaliyokuwa yakitolewa kuhusiana na hali za hatari kiroho? Hatuwezi amini ya kwamba malaika wale waliwaacha pasipo habari kamili kuhusiana na mitego ya Sodoma. Ni nini kilisababisha uharibifu huo wa kutisha wa roho kwa mwanamke huyu? Je, ilikuwa kwa sababu hakuamini mwito wa Mungu kuuondoka Sodoma?. Hapana. Hakuudhihaki ujumbe, kama walivyofanya binti zake waliokuwa wameolewa na waume zao. Aliamini onyo na hakika aliianza safari ya kuelekea mahali salama. Lakini zingatia hili—hakukuwa na hamu moyoni mwake na hakukuwa na shauku kwa ajili ya mpango wa kutoka. Alikuwa ni mtu wa kusitasita mno kuiacha miadi ya kupendeza iliyokuwa katika utajiri wa nyumbani kwao Sodoma kiasi kwamba alikawia.
Moyo na maisha yake yalikuwa yamefungamana na vitu vya duniani ambavyo ilikuwa vigumu kwake kuachana na hazina waliyokuwa wamejikusanyia ya nyumba zilizonakshiwa kwa ufahari. Mauti ikiwa inamnyemelea, alikawia. Pamoja na uzima na ulinzi vilivyokuwa vikimsubiri juu ya mlima, alikawia. Mwanamke huyu alikuwa na shida gani? Alipenda dunia zaidi ya vile alivyompenda Mungu. Bado alikuwa akiiamini kweli; alijua kile anachotakiwa kufanya; alitaka kuokolewa—walakini alikawia. Bado tunapata watu wengi sawasawa kama Bibi Lutu. Pia wanaiamini kweli, wanatambua kile wanachopaswa kutenda, na wanataka kuokolewa. Wanakawia, vile vile kama alivyofanya. Kama mke wa Lutu, wengi wao hukawia mpaka nguvu ya mvuto ya ulimwengu inatawala dhamiri kutenda, na wanakosa uwezo wa kuyaruhusu mambo ya ulimwengu yaondoke. Kwa nini watu watakawia kuitikia mwito wa Mungu? Je, umewahi kufanya?
Mamilioni wamekawia mpaka miaka ya fursa katika maisha yao inakwisha. Wanakawia hadi watoto wao wanakua na wanapotelea ulimwenguni. Wanakawia mpaka ulimwengu unawafunga kwa minyororo ya chuma na sauti ya Mungu kwao hufifia. Lakini hatimaye Bibi Lutu alianza kwenda. Kumbukumbu inaeleza jinsi malaika ilivyowabidi kuwashika mkono nyumba hiyo kuwaharakisha kuuondoka mji uliokuwa umetangaziwa maangamizo. Malaika walipaza sauti, “Jiponye nafsi yako usitazame nyuma” (Mwanzo 19:17). Lakini mkewe Lutu hakuifikia milima ya yenye usalama. Kwa nini? Biblia yatuambia kuwa ali—‘tazama nyuma,’ na papo hapo aligeuka kuwa nguzo ya chumvi. Kwa nini Mungu alishughulika naye kwa ukali kiasi hicho? Je, lilikuwa si kosa dogo tu kati ya yote kwa kugeuza tu kichwa chake? Neno la Mungu linalo jina la kukiita kitendo cha aina hiyo: dhambi. Alikaidi amri ya Bwana, na hukumu yake inakazia umuhimu wa utii. Mungu humaanisha kile akisemacho. Hakuna kisingizio cha dhambi, na Mungu hawezi kuipuuza.
Hawakuelewa uzito wa kukiuka utakatifu wa kile ambacho Mungu amekitenga kwa matumizi matakatifu. Hoja za kufanana zinatumika leo kwa uhusiano na mambo yaliyotakaswa na Mungu. Mara nyingi kumekuwa na swali, “Nini tofauti kati ya kuabudu siku ya Sabato na kuabudu siku ya Jumapili?—Siku moja ni njema kama ilivyo nyingine.” Utofauti mkubwa ni kwamba Mungu aliifanya siku moja kuwa takatifu na akaandika sheria isiyobadilika kuihusu hiyo kwenye mbao za mawe. Siku ya saba iko tofauti kwa sababu ina baraka za kipekee za Mungu juu yake. Ole kwa mtu azishikaye kwa mikono isiyotakaswa zile taasisi takatifu za Mungu. Nadabu na Abihu hawakuwa na hatia ya uasi wo wote kwenye imani yao katika maeneo mengine ya ofisi yao ya kidini. Hawakujali, wakikataa kutekeleza namna sahihi ya utoaji katika utaratibu ulioagizwa kupitia sheria za Kilawi. Suala dogo la moto lilikuwa hukumu hiyo tu iliyowapiga kama watu wasio makini na wasio na maana.
Kwenye eneo hilo tu, walijisikia wako sahihi katika kufanya badiliko dogo ambalo kwa urahisi na wepesi lingefaa kwenye mawazo yao ya kiutendaji wa ibada. Walifikiri kwamba uchepukaji huo mdogo katika matakwa ya shughuli hiyo takatifu kusingeleta matokeo yo yote makubwa. Bila shaka Mungu asingehesabu kuwa ni dhambi kufanya uboreshaji katika tendo la kumwabudu Yeye. Ni kinyume ilivyoje kwamba ukaidi mwingi wa sheria ya Mungu unatendeka katika jina la dini! Kristo alithibitisha kwamba watu wangemwabudu wakiwa wameweka “amri za wanadamu” kama mbadala wa matakwa Yake. Aliikataa ibada ya namna hiyo kama ni utupu na isiyofaa. Katika Hubiri mlimani, alieleza kundi kubwa ambao wangetafuta kuingia kwenye ufalme kwa visingizio vya kutoa unabii, kutoa pepo, na kutenda matendo ya kushangaza ‘kwa jina lako.’ Hata hivyo Yesu atawaambia, “Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu.” (Mathayo 7:23).
Ni kwa vipi watu wanakuwa vipofu na waliodanganywa kiasi hicho hata kujisikia amani kwamba wameokoka huku kwa makusudi wakivunja amri za Mungu? Katika ibada yao iliyo bure, mara zote walisujudu wakati wa maombi, kuimba nyimbo za sifa, na yawezekana hawakukosa hata kipindi cho chote kanisani. Walikiri upendo mkuu kwa Mungu na walitoa shuhuda za kusisimua za namna ile ile. Je, ni tatizo hilo hilo hata kwetu leo? Je, watu wenye dini bado wanakaidi sheria ya Mungu huku wakijidai kumpenda? Katika Sabato yo yote, tazama karibu yako kuona kile kinachoendelea. Watu watakuwa wakipuuza amri mahususi za msingi ambazo Mungu aliziandika kwenye mbao za mawe: “Siku ya saba ni Sabato ya Bwana Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote” (Kutoka 20:10).
Ni akina nani hawa wanaopuuza amri ya Mungu ya Sabato? Vile unavyowaona wakiharakisha kwenye shughuli zao za kila siku, wakifanya yawapendezayo wenyewe katika siku ya saba, kunaonekana hakuna shida katika kuvunja amri ya wazi ya Mungu. Lakini kesho, wengi wao watakuwa kanisani—wakiomba, wakiimba, na kusimuliana ni kwa kiasi gani wanavyompenda Yesu. Wamepata wapi kujua maana ya upendo? Je, ni kutoka kwenye mabango ya mtaani—“Tabasamu ikiwa unampenda Yesu,” “Punga mkono ikiwa unampenda Yesu,” “Piga kelele ikiwa unampenda Yesu,” Hicho si kile alichokisema Yesu, si ndivyo? Alisema, “Mkinipenda, mtazishika amri zangu” (Yohana 14:15).
Ndipo hutenda kama Sauli na kujaribu kuhalalisha ukaidi wao kwa kumwabudu Mungu katika jina la kile walichokiiba. Mungu alinena kupitia nabii Samweli, “kutii ni bora kuliko dhabihu.” Aidha, ni bora kuliko ibada zote zisizofaa zilizo katika maelfu ya huduma za kidini zinazoendeshwa kwa uhusiano na ukiukaji makusudi wa amri Yake bayana. Utii ni bora kuliko cho chote kile katika kufunua pendo letu. Ndivyo Yesu alivyosema. “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.” Ukaidi ni mbaya kuliko cho chote kwa sababu nit endo la uasi kwa asili yake bayana. Kutunza siku bandia iliyotokana na upagani wa ibada ya jua kamwe haikubaliwi na Mungu kama ilivyokuwa kwa ng’ombe na kondoo wa ushindi wa Sauli. Haheshimiwi kwa ukaidi, na hasa hasa anakoswa kwa uvunjaji wa amri Zake katika jina la ibada.
Umetambua kuwa katika visa vya Nadabu, Abihu, na Uza, kila kosa lililoonekana dogo sana lilipaswa kupatana na mambo ya Mungu aliyoyatenga kwa matumizi matakatifu? Moto ulikuwa mtakatifu, na sanduku la agano lilikuwa takatifu. Vyote vilipaswa kutunzwa na kuhifadhiwa kwa kusudi moja tu takatifu. Mikono michafu haikupaswa kugusa kwenye sanduku, na moto wa kigeni haukupaswa kuwa mbadala wa moto mtakatifu. Pale vile vitu vilivyo—“tengwa” vilipotendwa kama ilivyo kawaida ya mambo mengine, hukumu za Mungu zilishuka. Je, leo kuna mambo yaliyotakaswa ambayo Mungu ameyatenga kwa matumizi matakatifu? Kabisa yapo.
Sabato imeelezwa na Mungu kama “siku yangu takatifu” (Isaya 58:13, 14). Hiyo moja kati ya saba kwa heshima imebarikiwa na kuamriwa na Mungu kwa ajili ya pumziko na ibada. Zaka ni kitu kingine kilichotengwa kwa Neno la Mungu kwa makusudi mahususi na matakatifu. Kujitwalia hiyo moja ya kumi kwa ajili yetu wenyewe kwa hakika ni kumwibia Mungu. Maandiko yanaieleza hivi: “Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu.” (Malaki 3:8). Wengine wanashtushwa kusoma kuhusiana na hukumu zilizomwangukia Uza pale alipogusa sanduku la Mungu na kuhusiana na mkewe Lutu pale alipogeuza tu kichwa chake. Je, makosa madogo tu yanakuwa na ukali hivyo kiasi kwamba kifo cha papo kwa hapo hufuata?
Je, hii inadhihirisha kuwa kiasi cha dhambi si maana kama ilivyo dhambi yenyewe? Ikiwa tendo dogo la Hawa kula tunda lilipaswa kudumu kwa milenia sita za dunia-sayari ya kuteseka na kifo, hakika haifai kuthubutu kupima ukaidi kwa kutumia ukubwa au mwonekano. Haishangazi, kwamba mkewe Lutu alipatwa na matokeo ya kutisha yale yale kama wengine wote waliocheza na neno la Mungu mtakatifu. Kosa la kutazama nyuma liliashiria dhamira iliyogawanyika. Aidha, ilidhihirisha ukweli kwamba moyo wake bado ulikuwa umefungamana na mambo ya utaratibu mpotovu, uliolaaniwa wa jamii ile. Sauti mbili zilikuwa zinashindania utii wake: moja, sauti ya nyanda za juu—sauti ya Mungu ikimwita kwenye uhuru, usafi, na wokovu; nyingine, sauti ya nyanda za chini—sauti inayopendwa na wengi na ya anasa, sauti ya Sodoma.
Taratibu sauti toka chini ilitawala dhamiri iliyodanganywa, na Bibi Lutu anasimama mbele yetu kama mfano wa kuhuzunisha wa moyo uliogawanyika. Yesu alisema, “Mkumbukeni mkewe Lutu,” na alisema hivyo kwa wale ambao wangeliishi katika nyakati za mwisho za kustaajabisha za historia ya dunia. Anakisema kwetu sasa—“mkumbukeni mkewe Lutu.” Tunauhitaji ujumbe huo. Mamilioni wapo na mawazo yaliyogawanyika kama Bibi Lutu. Hawapati muda wa kuomba na familia yao. Kama Bibi Lutu, wengi husoma zaidi majarida kuliko Biblia, na hivyo wana dini ya juu juu tu. Kama Bibi Lutu, wanakawia waking’ang’ania dhambini na hawachukui maamuzi thabiti ya kuishi katika kumtii Mungu.
Hatima kali ile ile iliyotisha Sodoma imeamriwa pia kwa kizazi hiki cha uovu. Yesu alionyesha hali inayofanana kati ya vipindi viwili vya historia. Baada ya kueleza matendo mabaya na maendekezo kupindukia katika siku za Lutu, Yesu alisema, “Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu” (Luka 17:30). Alimaanisha nini kusema “hivyo ndivyo”? Je, ni matatizo yale yale ya kijamii na kimaadili? Bila shaka. Je, aliona mbele mvuto wa kushtua kwa akina Luku na Bibi Lutu wanaokawia ambao dhamira zao zimehafifishwa kwa kusitasita. Kabisa, lugha la Bwana inaonekana kudhihirisha kuwa mwonekano mzima dhalili wa dunia inayoangamia ulikuwa mbele Yake. Vile ilivyokuwa katika siku za Sodoma, watu watabaki na fursa moja tu ya mwisho kusema Ndiyo au Hapana; kisha itakuwa ndio mwisho.
Wengine, kama mkewe Lutu, watang’ang’ania ulimwengu kiasi kwamba watashindwa kuuondoka kwa wakati unaofaa. Wataangamia wakiwa na mambo waliyoyapenda zaidi kuliko walivyompenda Mungu. Wengine, kama Lutu, watainuka katika wakati mchache tu uliobakia kuchagua haraka na kufikia maamuzi. Bila kutazama nyuma, watakwenda kwa utii kamili kwenye mapenzi ya Mugu. Huu ni uchaguzi ambao kila mmoja unamkabili. Masuala yale yale yaliyoharakisha tukio la kushtua huko Sodoma yanaathiri makanisa ya kikristo karibu katika kila hatua. Tamaa ya mali na uvuguvugu yamebadili mtindo wa maisha wa mamilioni ambao wanakiri kuwa wafuasi wa ile kweli leo.
Wakati pepo za maangamizo zinapoondoka taratibu toka viganjani mwa malaika wanne watangazao maafa ambao wamekuwa wakizishikilia pepo hizo, watu wanaojidai ni wa Mungu wametulia katika ulimwengu ya mambo ya mwilini inayoonekana i salama. Kama familia ya Lutu, wameridhika katika jamii inayopenda mali na maridhiano kiimani. Mungu havumilii anapotazama muungano mchafu kati ya mwili na roho. Kama yule Shahudi Mwaminifu wa kanisa la Laodikia, awaita masalia wa siku za mwisho kutubu. Kama wale wajumbe wa kimbingu walivyotoa kauli ya mwisho miaka mingi iliyopita, vivyo hivyo twaitwa kuyaacha yote ama tuangamie. Hakuna muda zaidi wa kuwa na nia mbili. Ondoka, Mungu asema, na uwe moto au baridi. Toka uende ukaishi, ama baki u vuguvugu na uangamie.
Hakuna nafasi ya kujisalimisha nusunusu kanisani linalobadilishwa! Kisa cha Lutu na familia yake kinathibitisha kuwa Mungu hataendelea kuvumilia maisha ya nia mbili kwa upande wa watu Wake. Wale wanaojaribu kuishi katika dunia mbili sharti wafanye uamuzi. Neno la Mungu latangaza kuwa urafiki na dunia ni uadui kwa Mungu. “Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.” (Yakobo 4:4). Mwandishi mwingine, ambaye alikuwa mwanafunzi wa Kristo wa karibu zaidi, alitangaza, “Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake” (1 Yohana 2:15).
Lugha ngumu iyo hiyo ilitumiwa na Yesu katika kufafanua hali ile ile miongoni mwa viongozi wa kidini wa siku Zake. Aliwaita wanafiki, wana wa majoka, na wazandiki. Katika Agano la Kale, Mungu alitumia lugha ile ile katika kuwaita watu Wake waliokosa msimamo wajinusuru. “Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye” (1 Falme 18:21). Katika mifano hii yote, Mungu alikuwa akinena kwa wale ambao aliwatwisha dai la kuwa uchaguzi Wake na aliowapendelea. Hata hivyo, mtindo wa maisha haukuendana na upekee wao. Katika mapitio yao kulikuwa na maridhiano katika kitakatifu na cha kawaida. Walikuwa wakisema hivi na kutenda vile. Matokeo yake ilikuwa ni ushahidi usiona nguvu ambao haukuleta matokeo chanya kwa wengine.
Mungu aliona mwenendo huo kwamba unachukiza. Ndio maana alitaka chaguzi hizo zifanywe; lakini zingatia kuwa ni njia mbili tu zilikuwa zimetolewa. Ni ama Mungu ama Baali, utii ama ukaidi. Moja ya mgogoro mkubwa zaidi wa ukristo wa leo ni vile ilivyo rahisi kuchanganya dhana ya wokovu na dhambi. Biblia inaweka wazi sana kuwa uvunjaji wa kukusudia wa sheria ya Mungu ni kinyume na usalama wa kiroho. Wito wa Mungu ni ku—“toka kwake na kujitenga naye.” Ukaidi wa kudhamiria hauwezi ukapatana na dhamiri ya kikristo. Neno la Mungu lina mengi ya kusema kuhusiana na dhambi, lakini neno lo lote jema halina ila Biblia pekee. Hakuna aliyewahi kusoma maandishi rahisi yaliyovuviwa kwamba dhambi inapaswa kupunguzwa. Wakati wo wote inapotajwa, dhambi inatangazwa kuwa haina mjadala.
Inapaswa kuachwa, kukataliwa kata-kata. Yesu hakusema kwa mwanamke mzinzi, “Nenda na upunguze kutenda dhambi hii.” Alisema, “Nenda na usitende dhambi tena.” Yohana hakuandika: “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba mtende dhambi kidogo kidogo.” Alitangaza wazi, “nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi.” Kisa cha mkewe Lutu ni ufafanuzi wa kuvutia kwamba uwepo wat endo moja dogo la ukaidi wa kukusudia laweza kupelekea upotevu milele. Jitihada yo yote kupatanisha pendo la Mungu, tabia, au haki kwa kuendekeza dhambi lazima mwisho wake uwe ni kutofaulu kulivyo vibaya. Hili kwako likoje? Katika kipande hiki cha mwisho cha rehema, je, umemwacha kila mshindani wa Kristo kuwa nafasi ya kwanza katika moyo wako? Vile ilivyokuwa kwa Malaika kumsihi Lutu na nyumba yake kujisalimisha kikamilifu, Roho Mtakatifu anatuhimiza kujitoa vivyo hivyo leo.
Wito ni kujitenga na uamuzi wa haraka. Watu wengi wanakawia katika kusitasita wakati wa machweo ya jua huku mioto ya maangamizo ikiwekwa tayari kuteketeza dunia hii. Walimwengu na Wakristo, wote wanasikia ombi la Mungu kumrejea Yeye. Mlango wa rehema bado u wazi kwa muda mfupi sana. Kwa kila nafsi kuna wasaa wa mwisho adhimu kufanya maamuzi kabla mlango haujafungwa. Je, wote wataweza kuutambua wasaa huo? Cha kusikitisha, hapana si wengi. Wengine, wakiwa na fahamu zilizohafifishwa kwa maridhiano ya kidunia, hawatapambanua hata kuondoka kwa mjumbe wa Mungu wa wokovu. Leo dhambi za Sodoma zinapumbaza na kutamanisha kama zilivyokuwa zamani. Mitindo ile ile potofu imekuwa kawaida na inayopendwa na wengi zaidi kuliko ilivyokuwa katika mji ulikuwa umeandikiwa maangamizi katika nyanda za tambarare. Lutu hakuwa na fursa ya kuchukua cho chote.
Ndivyo kwetu inavyopaswa kuwa. Lazima kuwepo na utayari kujikana nafsi na kuachana na machukizo ya tamaa za mwili katika kila namna. Tumaini letu pekee ni kuharakisha kujitenga na maovu ya jamii iliyopotoka. Mwokozi atupendaye asimama mlangoni akisema, “Tokeni kati yao, mkatengwe nao, asema Bwana.” Siri ya kuweza kupinga na kukataa mivuto ya jamii potofu na asi ni kutazama msalaba wa Yesu Kristo. Twaweza kukereka na uovu na kuwa na shauku ya kuokolewa, lakini kuna chanzo kimoja tu cha nguvu kuuvunja mkondo wa dhambi. Kifo cha Kristo pale Kalwari, ambapo ilikuwa adhabu yetu, kilitimiza dai ambalo uasi ulikuwa umeliweka dhidi ya kila roho ulimwenguni. Sheria iliyovunjwa ilidai kifo, na pale Yesu alipoteseka adhabu hiyo kwa kila mwanadamu msalabani, biashara tukufu ilifanyika.
Pale msalabani Kristo alijitoa kwa ajili ya mbadilishano wa kuvutia mno. Alijitoa ili kujitwika hatia na shutuma za kila mdhambi tangu mwanzo wa wakati. Na cha kushangaza zaidi, alikubali kupokea matokeo yote ambayo matendo yale ya giza, yasiyoneneka, yalikuwa yameathiri wale wadhambi wanaotaabika. Je, waweza kupima kujitoa huko na jinsi kusivyo na ubinafsi? Na nini alitoa kama mabadilishano kwa yale mawazo mabaya ya aibu na hatia? Kwa kila mmoja ambaye angeikubali, Kristo alijivika usafi wake wa maisha Yake matakatifu ya utii. Kwa njia ya imani nyofu, mabaya yaliyokwisha pita hata ya mhalifu asiyestahili yanaweza papo hapo kufunikwa kwa haki kamili. Wakiwa wamevikwa ndani ya vazi hilo lenye sifa ya ukamilifu, waamini wote wanaweza kuhesabika kwa Mungu kana kwamba hawakuwahi kutenda dhambi. “Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu” (Isaya 1:18).
Paulo alieleza uzoefu wa yule anayedai kuhesabiwa haki kwa njia ya Imani katika damu Yake. Aliandika: “wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa MUNGU dhambi zote zilizotangulia kufanywa. Apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu.” (Warumi 3:24-26). Hapa kwa dhahiri inafunuliwa sura ya ukubali wa mtu mmoja mmoja wa wale wanaokiri kuwa Yesu ni mtoa msamaha na atupatiaye haki. Ni nini kimetimizwa kwa wale wanaoingia katika mahusiano ya karibu zaidi na kuhesabiwa haki kwa imani?
Je, wanaokolewa toka hatia ya dhambi peke yake, au pia huokolewa toka katika dhambi yenyewe? Paulo alilijibu swali hilo. “Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu” (Wagalatia 6:14). Katika fungu hili tunapata kuwa ushindi juu ya mfumo mwovu wa ulimwengu umefungamana haswa na upatanisho wa msalaba. Hakuna aliyeokolewa toka dhambini pasipo kupokea ukombozi huo kama zawadi kwa njia ya stahili ya mateso ya Kristo na kifo. Tunafanywa kuwa wafu kwenye mivuto ya dunia kwa kutazama usoni pa Mbadala na Mwokozi wetu.
Pendo lake la Agape, lililofunuliwa pale msalabani, huyeyusha ukaidi na huuweka mbali moyo dhidi ya kila mvuto ambao ulimwengu waweza kuubuni. Ndivyo Yesu alivyo— “fanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi” (1 Korintho 1:30). Yote ni msalabani. Utazame kila siku na mkumbuke mkewe Lutu, ili uokolewe toka katika adhabu ya mwisho ya kutisha.